

TV ya INJILI Kwenye Internet
-
WWW.GOSPELGTV.COM
Tel.
254722602445 E-mail:
munishi@munishi.com or info@munishi.com
Polisi
Kenya wamuua Matheri

Polisi nchini Kenya wamemuua kwa kumpiga risasi kisogoni Matheri
waliyemwita Jambazi sugu na hatari. Pichani ni Matheri kabla na baada
ya kuuawa. Pamoja naye ni mwanamke ambaye hakuweza kujulikana jina
lake. Aliuawa pamoja na Matheri. Inaonekana kwamba Polisi walimfunga
mikono nyuma kabla ya kumuua nje kidogo ya nyumba yake baada ya kujisalimisha.
Walifanya shambulio hilo
usiku wa manane nyumbani kwa Mtuhumiwa huyo, baada ya kujisalimisha
kulingana na mkewe.Akionge na camera za TV baada ya tukio, Mkewe Matheri
alisema kwamba Polisi waliizingira nyumba yao na kumwamuru Matheri
ajisalimishe au waichome moto nyumba yao. Baada ya Polisi walibadili
tishio lao na kusema wangeimiminia nyumba yote risasi kupitia madirishani.
Ndipo mke wa Matheri alipomsihi ajisalimishe ili awanusuru watoto
na Matheri alikubali bila swali. Aliongeza kwamba baada ya kuhojiana
na polisi huko nje kwa zaidi ya nusu saa, mama huyo alisikia kukurupushani
na baadaye milio ya risasi jambo lililomuashiria kwamba mume wake
awezakuwa amejeruhiwa vibaya au awe amekufa.

Hawa ni mke na watoto wa marehemu aliyebandikwa jina la Jambazi
sugu Kenya. Inawezekana kuna ukweli fulani katika tuhuma hizo, lakini
kwa hawa watoto Matheri alikuwa baba aliyekuwa anakutana na mahitaji
yao. Wapiga picha wetu walikuta mabaki ya chapati na kitoweo cha nyama
ya kuku jambo linaloashiria kwamba Matheri alikula chakula cha jioni
na jamii yake, asijue Polisi watauchukua uhai wake usiku huo.
INdivyo ilivyo hakuna
aijuae siku wala saa ya kuja kwake Yesu mwana wa Mungu. Ndiyo maana
tunawaonya majambazi wote watubu na waziache njia zao mbaya kwani
wasipofanya hivyo hakuna wa kuwarekebisha kwani hata Polisi wameamua
kupoteza ubinadamu nao wanafanya kama majambazi wafanyavyo. Majambazi
wanaua na Polisi wanaua. Tofauti yao ni gani?

Hata NDOVU hawezi kuwindwa na Polisi wengi hivi. Lakini nani hasa
aliyeamua kwamba ni heri kuyamaliza maisha ya Matheri kuliko kumpeleka
gerezani akaone TV na kucheza mpira baada ya makamu wa Rais Mudy Awori
kuyafanyia ukarabati magereza ya Kenya. Je sasa sheria za utaratibu
wa mahakama umewachosha Polisi wetu kufikia kuamua kuwaua wahalifu
hata pale wanapojisalimisha?
Dunia hii ya Mungu tutaona
Mengi kabla Yesu kurudi. Wanyama wa porini hawana sheria wala mahakama.
Kuuana na kuchinjana ni mtindo wa maisha mazima mwituni. Lakini kuna
ndege ambao huwa hawapendi kuona damu ikimwagika kila siku. wanachofanya
ni kupiga kelele wanapowaona simba wakilikaribia kundi la swala. Wakisikia
maonyo wanakimbia kabla wakutwe. Wakipuuza shauri yao watajilaumu
wenyewe. Nasi tumechoshwa na umwagikaji wa damu kila siku kila mahali
duniani. Tunachofanya hapa ni kupiga kelele ili wanadamu wote waukimbilie
usalama kwa Mungu wao. Vinginevyo shetatani amewaingia wanadamu na
wanafanya kama wanyama. Ubinadamu umewatoka. Kimbieni kwa Mungu kwa
njia ya kutubu dhambi na kumwamini Yesu ili dhambi zenu zisamehewe
na majina yenu yaandikwe kwenye kitabu cha uzima.

Mzazi wa Matheri baada ya kuburuzwa chumba cha maiti kuutambua
mwili wa mwanae. Inasemekana hakuongea. Haijalishi walimwita nani,
lakini kwake ni mwanae, na uchungu wa mwana aujuae ni mzazi.
Kila mzazi hajui anazaa
nini. Rais karani, Daktari wote huzaliwa. Hakuna anayependa kuzaa
jambazi. Lakini ikitokea uwe ulizaa jambazi kosa hapo linakuwa la
nani? Mbona nasikia mzee huyu amepokea kipigo kutoka majirani mara
nyingi na hata wamemchomea nyumba? iweje makosa ya mtoto aathibiwe
mzazi? tena bila kuufuata mkondo wa sheria? Tulichokiona asubuhi ya
kuuawa kwake huyo waliyemwita jambazi mkuu Kenya, hakikufurahisha,
kinatisha na hakipaswi kurudiwa. Jamii ikikosa mwelekeo ianze kufurahia
mauaji ni kinyume na amri za Mungu. Kuua ni kazi ya Mungu na hakuna
mwanadamu anayeruhusiwa kufanya hivyo kwa sababu zozote. Akitokea
mwanadamu aliyepotoka kiasi cha kuondokewa na ubinadamu wake aanze
kuua, wale walio na ubinadamu bado wanapaswa kufanya kila linalowezekana
kumrudisha huyu aliyepotoka katika maadili sahihi ya ubinadamu. Kuua
haijawahi kuwa suluhisho. Tena haiwezi kuwa adhabu maana kila mtu
atakufa. Utamwadhibuje mtu kwa kile kitakachokupata hata bila kufanya
kosa? Bunduki na mlio wake mkali haijawahi kutatua matatizo duniani.
Tena haitawahi wala msitegemee kwamba siku moja mtutu wa bunduki utamaliza
ujambazi duniani. Kitendo cha polisi kummiminia risasi Matheri baada
ya kujisalimisha na kisha kumburuza baba yake mzazi akaione maiti
ya mwanae, hicho hakikuwa kitendo cha kibinadamu. Tunakilaani kwa
nguvu zetu zote. Hakuna mtu anayeunga mkono ujambazi. Pia hatuifurahii
kazi ya majambazi. Polisi wanaposema Matheri ndiye jambazi nambari
wani Kenya, wanapaswa kuthibitisha hilo. La sivyo Matheri atabaki
kuwa mtuhumiwa wa ujambazi aliyeuawa baada ya kujisalimisha kwa Polisi.
Kitendo hiki kitaichonganisha jamii na Polisi kuliko na majambazi.
Sababu7 ni kwamba Matheri wanayesema aliua, hatukumuona akiua, lakini
tumewaona Polisi wakimuua. Kwa watoto wa Matheri waliowashuhudia Polisi
wakimmiminia risasi baba yao, Kwao haitafutika kwamba Polisi ni wauaji.Inasemekana
kwamba mkewe Matheri alimtaka ajisalimishe ili kumnusuru yeye na watoto,
jambo ambalo Matheri alikubali bila swali. Hii inaonyesha huyo waliyemwita
Jambazi hatari, alikubali kujitolea kwa polisi kuepusha waliokuwa
wakiitafuta roho yake wasiwadhuru watoto. Je baada ya kumuua Matheri
haki itawahi tendewa wanaodaiwa kuuawa na Matheri? Je Ujambazi Kenya
utamalizika na wakenya walale milango wazi? Hayo ndiyo maswali polisi
walipaswajiuliza kabla ya kufyatua risasi kumwelekezea Matheri na
mwanamke wanayedai alikuwa msaidizi wake. Na kweli Polisi haikuona
umuhimu wa kumwacha hai huyo mwanamke awasaidie kuwakamata majambazi
wengine? Kama wote wawili walijisalimisha kama magazeti yote Kenya
yalivyoripoti, kwa nini kuwaua? Katika suala hili tunawapongeza Media
kwa kufanya kazi nzuri. Panapokosekana Polisi na Mahakamazinazofuata
maadili ya kazi yao, isikosekane Media inayoripoti ukweli kama ulivyo
hata kama wengine hawataufurahia. Mbona Polisi walimkamata mkewe Matheri
baada ya kuwasimulia wanamedia kwamba mumewe aliuawa baada ya kujisalimisha?
Je walitaka story hiyo iripotiwe vinginevyo? Kwa upande wao Polisi
walimhusisha Matheri na mauaji Mengi nchini Kenya, yakiwemo yale ya
Wamarekani wawili waliouawa karibuni mjini Nairobi. Nao Amerika wamesisitiza
kuendelea na uchunguzi wao kuhusu kilichosababisha mauaji ya raia
wao, huku wakikataa kuamini kwamba yalisababishwa na Matheri kama
Polisi wanavyodai. Kuna wanaoamini kwamba kusakwa na hatimaye kuuawa
kwa Matheri kulichangiwa sana na mauaji wa Wamarekani na siyo vita
halisi ya ujambazi unaowasumbua Wakenya. Picha nyingine inayopatikana
katika sakata hili ni kwamba Polisi wanawajua majambazi wote, na mmoja
anakuwa hatari wakati anapotofautiana na baadhi yao katika mgao. Ni
siri iliyo wazi kwamba visa vingi vya ujambazi Afrika vinahusisha
baadhi ya wana vikosi vya usalama. Kuna wanaodai kwamba Polisi wakiwania
kumaliza ujambazi inawezekana kama wataanzia na wao wenyewe. Lakini
mambo yalivyo sasa ni kwamba kila jambazi anapaswa kujiuliza mara
mbili kabla ya kushirikiana na polisi kufanya ujambazi. Mambo yakienda
mrama usulubishwe, hata kama utajisalimiosha itabidi shaba iingie
mwilini mwako ili usiwaseme maofisa unaoshirikiana nao. Je ukweli
huu utafichwa kwa muda gani? Tunashukuru kwamba Media Nchini Kenya
wameanza kuchimbua kuelekea kuupata ukweli unaofichwa mara nyingi
katika watuhumiwa wanaouawa baada ya kujisalimisha. Sambamba na hilo
tunalaani kwa nguvu zote watu wanaoacha kufanya kazi kwa jasho lao
na kujihusisha na vitendo vya ujambazi. Mbaya zaidi wanawaua wanaowaibia
mali zao. Huo siyo ubinadamu. Watu kama hao wanapaswa kuibadili mienendo
yao na kufanya kazi kwa mikono yao wajipatie riziki badala ya kuwa
majambazi. Majambazi wakifanya makosa na Polisi wafanye makosa, Media
wakisema ukweli wakuu wa dini tunapaswa kuwapongeza wakweli. Katika
hili tunawapongeza Media Nchini Kenya na tunawataka wengine barani
Afrika waige mfano wao mzuri.