Kimurgor Ameuawa



Aliyekuwa Mlinzi mkuu wa Moi Bwana Kimurgor,
ameuawa mjini Nairobi. Commando aliyesomea Israel, pia aliwahi kuwa
mkuu wa kikosi cha GSU wakati wa utawala wa Rais mstaafu Moi. Wakati
serikali ya Kibaki ilipochukua madaraka, Bwana Kimurgor alistaafishwa
na kuwa raia wa kawaida. Mpaka siku ya kufa kwake, alikuwa ofisa
ulinzi katika kampuni binafsi ya ndege. Inasemekana kwamba alikuwa
akiendesha mwenyewe ndani ya gari yake aina ya TOYOTA PRADO katika
mtaa wa Fedha Estate, alipokutana na watu watatu wenye silaha.Aliposimamishwa
na watu hao, alihisi hatari na kukaidi amri yao. Aliendesha kasi
kuwapita lakini commando safari hii hakuwa na bahati kwani walimfyatulia
risasi zilizoyakatiza maisha yake papo hapo.Polisi wameanza msako
mkali, huku vyombo vya habari vikiripoti kwamba wauaji wake walikuwa
majambazi wa kawaida. Ila hakuna chochote kilichoibiwa kutoka kwa
marehemu. Hata silaha yake aina ya pisto ilikutwa ikiwa sawa na
risasi kumi na moja ndani yake, jambo linaloonyesha kwamba commando
hakuweza kuitumia silaha yake kujikinga na watu waliopania kumuua.


Nchi za Kiafrika marais hulindwa na watu kutoka Kabila lao kama
siyo ndugu zao wa kuzaliwa.Hata kama hawana taaluma hiyo ya ulinzi,
Pesa za Serikali hutumika kuhakikisha wamepata mafunzo husika. Rais
akiachia madaraka basi walinzi wote wa rais hufutwa kazi kama siyo
kuuawa. Ikiwa madaraka yalichukuliwa kwa nguvu, basi walinzi wote
wa rais hukimbilia uhamishoni kwani wanakijua kinachowangoja. Hiyo
ndiyo Afrika yetu. Badala ya kuwafundisha wazalendo wanataaluma
ya ulinzi bila kujali kabila lao, usishangae hata mkuu wa majeshi
katika nchi nyingi za Kiafrika lazima atoke kabila la Rais au awe
ndugu wa karibu.Nani aliwadanganya Waafrika kwamba ndugu wa karibu
hawezi kuwageuka? Tena nani aliwapotosha kwamba watakuwa salama
mikononi mwa watu wa kabila lao? Siyo ajabu viongozi wengi Afrika
hawataki kutoka ikulu wakishaingia.Wanahitaji miaka mingi kuweza
kuwaandaa ndugu zao waweze kushika nyadhifa zote muhimu katika nchi.Wakitoka
madarakani, Yule atakaeingia haijalishi amesoma kiwango gani, Bado
atafuata utamaduni huo huo wa kijinga. Kubadili wakuu wote wa vikosi
vya ulinzi, Hata jaji mkuu lazima atoke karibu na kijijini kwao.
Usiwahi kutegemea haki katika vyombo vya sheria Afrika. Inategemea
unamjua nani. Nasikia hata nchi zilizoendelea mambo hayatofautiani
sana na Afrika. Badala ya Ukabila, wao wanatumia matabaka na kwingine
ubaguzi wa rangi Wakati mwingine dunia inaweza kuwa chungu sana
hasa ukiwa na mawazo huru yasiyoegemea upande wowote.


Wanahabari nao hawakuachwa nyuma katika
uoza huu. Serikali nyingi Afrika huakikisha zina ajenti wao katika
kila chombo cha habari nchini .Ndiyo maana vitendawili haviishi
kila kukicha. Utasikia "fulani ameuawa na majambazi wa kawaida,
baada ya kuwakuta wameshampora gari mama mwingine, na walipotaka
kutoroka wakitumia gari ya marehemu; inaonekana marehemu alikaidi
amri ya majambazi hao wa kawaida; na ndipo walipomfyatulia risasi
na kumuua, bila kuchukua chochote. Hata Bunduki ya marehemu haikuchukuliwa.
Tunawaomba wanainchi muwe watulivu kwani serikali haihusiki kabisa
na mauaji hayo ila ni majambazi wa kawaida."
Swali ambalo mtu anaweza kujiuliza
ni, Ilikuwaje vyombo vya habari vikawa vinawajua majambazi wa kawaida
na wale wasio wa kawaida? Je nchi inapaswa kuwa na hao majambazi
wanaoitwa wa kawaida? Mbona wanatuarifu kana kwamba wanataka ushahidi
fulani uonekane? Yaani wamekazania majambazi wa kawaida, kana kwamba
serikali haiwezi kutayarisha mauaji yaonekane watakavyo. Katika
nchi za Kiafrika tumeona mengi.Tumewaona viongozi waliouawa na kisingizio
kikawa ni ajali za barabarani. Wengine walipewa sumu na kisingizio
kikawa ni shinikizo la moyo. Wengine walipelekwa ngambo na walipouawa
huko, kisingizio kikawa ni maghaidi na wauza madawa ya kulevya waliommaliza
baada ya kuwatapeli.
Mambo ni mengi. Na wanasiasa husema
njia za kuua panya ni nyingi. Tunaomba isiwe kwamba Kimurgor naye
amemalizwa kwa moja ya njia hizo.

